JK apewa tuzo ya usalama wa chakula

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyotolewa Dar es Salaam, Tuzo hiyo imetolewa na Taasisi ya Mtandao wa Kutathmini Sera za Kilimo na Maliasilik (FANRPAN) katika hafla maalumu iliyofanyika juzi jioni wakati wa mkutano wake wa mwaka unaofanyika Dar es Salaam.

Ilisema Rais Kikwete anakuwa kiongozi wa tano wa Afrika kupokea Tuzo hiyo ambayo kwa lugha ya Kiingereza inajulikana kama Food Security Policy Leadership Award tangu kuanzishwa kwa Tuzo hiyo mwaka 2008 wakati ilipotolewa kwa aliyekuwa Rais wa Malawi, Bingu Wa Mutharika.

RAIS Jakaya Kikwete ametunukiwa Tuzo Maalumu ya Sera za Usalama wa Chakula na Uongozi katika sekta ya kilimo, ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wake na uongozi wake katika sekta hiyo.

Wengine waliowahi kutunukiwa Tuzo hiyo ni Rais Armando Guebuza wa Msumbiji mwaka 2009, Rais Hifikepunye Pohamba wa Nambia 2010 na Malkia, Mama wa Mfalme Ntombi, Indlovukazi wa Swaziland.

Akizumgumza kabla ya Rais Kikwete kukabidhiwa Tuzo hiyo, Mtendaji Mkuu wa FANRPAN, Dk Lindiwe Sibanda alimwelezea Rais kuwa ni bingwa mtetezi na kiongozi shupavu wa sekta ya kilimo katika Tanzania na barani Afrika. Mama huyo alisema:

“Mheshimiwa Rais wewe ni bingwa. Unatanguliza mahitaji ya watu wako mbele kama vile unavyofanya katika sekta ya kilimo ambayo ni tegemeo la watu wengi katika Tanzania na Bara letu. Kupitia mipango yako ya kilimo, kamwe Tanzania haitakuwa ile ile ambayo uongozi wake uliupokea mwaka 2005. Kamwe Tanzania imebadilika sana chini ya uongozi wako.” Dk Sibanda aliongeza:

“Kwa hakika umefanya mengi siyo kwenye kilimo tu, bali kwenye kusimamia amani na usalama, katika kukuza uhuru wa kila aina, katika masuala ya afya, elimu, miundombinu na maendeleo ya vijana.”

Hata hivyo, Dk Sibanda alitoa changamoto tatu kwa Rais Kikwete ambazo ni kumtaka aongeze maradufu matumizi ya mbolea kwa wakulima kutoka kilo 10 za sasa kwa hekta hadi kufikia kilo 25 ifikapo 2015.

Alimtaka kuhakikisha anaongeza maradufu uzalishaji wa mazao ya kilimo na hasa kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwa sukari ifikapo mwaka 2015 na tatu kuwashirikisha wakulima wadogo katika uzalishaji mbegu. “Tutarudi tena Mheshimiwa Rais mwaka 2015 kuyatazama tena upya mambo haya matatu.”

Akizungumza baada ya kupokea Tuzo hiyo, Rais Kikwete aliwapitisha washiriki wa mkutano huo kwenye hatua zote ambazo Serikali yake inachukua kupambana na changamoto zote zinazokifanya kilimo cha Tanzania kubakia kwenye uduni, ikiwa ni pamoja na kuongeza maeneo ya umwagiliaji, matumizi ya mbegu bora, matumizi ya dawa za kuua wadudu, matumizi ya mbolea nyingi zaidi, uboreshaji wa miundombinu ya barabara vijijini, uimarishaji wa vikundi vya ushirika wa uzalishaji na upanuzi na uimarishaji wa masomo.

Aidha, Rais aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa Serikali yake iko mbioni kuanzisha Soko la Mazao kama namna ya kuwawezesha kwa uhakika wakulima kwa kuhakikisha wanapata bei nzuri ya mazao yao.

Date: 
Wednesday, September 19, 2012
Source: 
habarileo
Category: 
Related news