LIGI YA VODACOM YAINGIA RAUNDI YA PILI

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya pili kesho (Septemba 19, 2012) kwa timu zote 14 kuumana katikaviwanja saba tofauti nchini.Wakati Simba ikiwa mgeni wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa Yanga kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro. Viingilio kwa mechi ya Uwanja wa Taifa vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 wakati kwenye Uwanja wa Jamhuri itakuwa sh. 3,000 kwa sh. 10,000. Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazochezwa kesho ni African Lyon vs Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam. Nayo Ruvu Shooting itashuka kwenye Uwanja wake wa Mabatini, Mlandizi kuikabili Mgambo Shooting kutoka Handeni mkoani Tanga.Tanzania Prisons itakuwa kwenye Uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuisubiri Coastal Union ya Tanga wakati Oljoro JKT itaitembelea Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza utashuhudia mechi kati ya wenyeji Toto Africans na Azam.

Date: 
Wednesday, September 19, 2012
Source: 
janejohn5
Category: 
Related news